Historia

Nia ya kuendeleza tasnia ya nyama ni tukio la kihistoria, zamani kabla ya uhuru wa Tanganyika, Serikali ilitoa mamlaka ya kusimamia maendeleo ya tasnia ya nyama kwa Kampuni ya Tanganyika Packers Limited (TPL). Mamlaka hayo yalikoma mara baada ya Kampuni hiyo kubinafsishwa mwaka 1974. Baada ya hapo, tasnia ya nyama iliwekwa chini ya Mamlaka ya kuendeleza Mifugo (LIDA) kisheria ambayo ilianzishwa kwa sheria Na. 13 ya Mwaka 1970 kama kampuni mama ikiwa pamoja na kampuni tanzu za:-

1. Kampuni ya Taifa ya Chakula Barafu (NCCC), iliyoshughulikia uhifadhi, usafirishaji na miundombinu ya baridi wakati wa mauzo ya rejareja ya nyama na bidhaa za nyama ndani na nje ya nchi .

2. Kampuni ya Masoko ya Mifugo (TLMC) iliyoshughulikia masuala ya masoko/minada ya mifugo

3. Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) inayojishughulisha na uzalishaji wa nyama ya ng’ombe katika ranchi kubwa

4. Kampuni ya Mashamba ya Ng’ombe wa Maziwa (DAFCO) iliyojishughulisha na uzalishaji wa maziwa

5. Kampuni ya Maziwa Tanzania (TDL) iliyojishughulisha na ukusanyaji, usindikaji, masoko na usambazaji wa maziwa na bidhaa za maziwa

6. Kampuni ya Taifa ya Kuku (NAPOCO) iliyojishughulisha na uzalianaji, utotoleshaji na uzalishaji wa kuku wa mayai na nyama

7. Kampuni ya vyakula vya Mifugo (TAFCO) iliyojishughulisha na uzalishaji na uchanganyaji wa vyakula vya mifugo

8. Kampuni ya Ngozi Tanzania (THS) iliyojishughulisha na maendeleo ya tasnia ya ngozi kwa kuboresha uzalishaji, usindikaji na masoko ya ngozi

9. Kampuni ya Ufungashaji ya Tanganyika (TPL) iliyojishughulikia usindikaji wa nyama

Hata hivyo, Serikali ilifuta sheria iliyoanzisha LIDA na hivyo kufilisiwa. Kampuni ya ufungashaji ya Tanganyika (TPL) iliendelea kufanya kazi mpaka mwaka 1993 ilipofungwa. Kati ya mwaka 1993 na 2000, wakati ambapo kampuni hizo zilikuwa zimefungwa, tasnia ya nyama iliendelea kufanya kazi katika mfumo usio rasmi na bila usimamizi wowote.

Mwanzoni mwa miaka 2000, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa tasnia ya nyama waliona umuhimu wa kufufua tasnia ya nyama na kuendesha mkutano wa wadau wa sekta ya mifugo uliofanyika Arusha kati ya tarehe 2 na 4 mwezi Aprili 2001, chini ya uwenyekiti wa aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu Mheshimiwa Benjamin W. Mkapa. Mkutano huo uliainisha changamoto na kupendekeza namna bora ya kuzikabili kuwa fursa. Miongoni mwa changamoto zilizoainishwa ni pamoja na usindikaji wa mazao ya mifugo ,soko na kubaini kwamba uongezaji mdogo wa thamani kwenye mazao ya mifugo unaoelezwa kwa kutokuwepo kwa upangaji wa madaraja ya mifugo na mazao yake. Pia, kutokuwepo kwa miundombinu ya usindikaji, huduma zilizo chini ya kiwango , ufungashaji wa mazao ya mifugo, bei kubwa ya vifungashio na usimamizi hafifu, Aidha, elimu na ujuzi mdogo miongoni mwa wadau wa mnyororo wa thamani wa mifugo vilionekana kuchangia ufanisi mdogo wa sekta ya mifugo.

Kwa upande mwingine, masoko ya mifugo, mazao ya mifugo na biashara kwa ujumla inakabiliwa na vikwazo vingi ambavyo ni pamoja na:-

  • Miundombinu dhaifu ya masoko ya mifugo na mazao yake
  • Udhaifu wa mfumo wa usafirishaji wa mifugo na mazao yake
  • Kutokuwa na taarifa za kutosha za masoko ya mifugo na mazao yake ndani na nje ya nchi
  • Udhaifu wa vyama vya wadau ambavyo husababisha kutopatikana kwa bidhaa nyingi za kutosheleza mahitaji ya soko
  • Uratibu duni miongoni mwa wadau wa mnyororo wa thamani wa mifugo
  • Ukosefu wa elimu na ujuzi wa ujasiriamali ikiwa ni pamoja na ushawishi
  • Ushindani kutoka nchi zinazouza mifugo nje ya nchi kwa masoko yaliyopo na masoko mapya
  • Kuzalisha kwa kuzingatia kanuni za biashara ya mifugo za kimataifa
  • Kuwepo kwa vikwazo vya biashara hususan vikwazo visivyo vya kodi ikiwa ni pamoja na zuio katika kuingiza mifugo hai na mazao ya mifugo
  • Ushindani unaotokana na bidhaa zilizozalishwa katika nchi zinazofidia gharama za uzalishaji ambazo zinarudisha nyuma wawekezaji

 

Mkutano huo uliazimia kuimarisha usimamizi katika sekta ya Mifugo kwa kufufua na kuweka usimamizi wa sekta ya mifugo na hivyo kutunga Sera na Sheria mbalimbali zinazosimamaia sekta ya Mifugo kama vile Sera ya Taifa ya Mifugo ya mwaka 2006, Sheria ya Magonjwa ya wanyama Na. 17 ya Mwaka 2003, Sheria ya Veterinari Na. 16 ya Mwaka 2003 na Sheria ya Nyama Na. 10 ya Mwaka 2006 pamoja na sheria nyingine zinazosimamia sekta ya mifugo. Baadhi ya sheria hizi zilianzisha taasisi kwa lengo la kuimarisha usimamizi katika sekta ya Nyama .

Bodi ya Nyama Tanzania ni Taasisi ya Serikali iliyoundwa chini ya Kifungu Na. 8 cha Sheria ya Nyama Na.10 ya Mwaka 2006 na kuzinduliwa tarehe 14 Novemba, 2008 na Mhe. Dkt John Joseph Pombe Magufuli (Mb) aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi. Kwa mujibu wa Sheria hiyo, Bodi imepewa mamlaka ya kuijenga upya tasnia ya nyama kwa kuweka misingi madhubuti ya kiutawala na kuhakikisha uzalishaji, usindikaji na biashara ya nyama na bidhaa zake unazingatia viwango vya ubora ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje.