Wizara ya Mifugo na Uvuvi Tanzania kupitia Idara ya Huduma za Mifugo (DVS) imekubaliana na Bodi ya Nyama Tanzania (TMB) kusimamia vibali vya kuingiza na kuuza nje nyama na bidhaa zake katika mipaka yote nchini.
Makubaliano hayo yamefikiwa katika kikao kati ya TMB na DVS kilichofanyika Septemba 18, 2024 jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa kikao hicho, Meneja wa Idara ya Ufundi kutoka TMB Bi. Afsa Milandu akifungua kikao hicho amesema, Wafanyabiashara ya nyama wa kuingiza na kuuza nje ya nchi wanatakiwa wawe na Vibali kutoka TMB na DVS vya kuwawezesha kufanya kazi hiyo na ili kuepusha vibali hivyo kutumika mara mbili ni lazima kibali kifungwe baada ya kutumika.
Bi. Milandu amesema “jukumu la kukagua na kufunga vibali vya TMB linafanywa na watumishi wa Idara ya DVS kutokana na uhaba wa watumishi wa TMB katika mipaka yetu nchini”
Aidha, katika kikao hicho TMB imeshauriwa iongeze muda wa vibali kutoka siku saba hadi 28 ili kumuepusha mfanyabiashara kuhuisha mara kwa mara anapoandaa bidhaa zake kabla ya kuzisafirisha.
Kikao hicho kilichofanyika kwa njia ya zoom kilishirikisha watumishi kutoka Bodi ya Nyama Tanzania, Idara ya Huduma za Mifugo na Ofisi za Kanda za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi.