WATUMISHI BODI YA NYAMA TANZANIA WAPIGWA MSASA
Watumishi wa Bodi ya Nyama Tanzania (TMB) wapatiwa mafunzo juu ya Rushwa, Afya ya akili na Virusi vya UKIMWI na UKIMWI ikiwa ni utaratibu wa kila mwaka kwa watumishi wa Bodi hiyo kukumbushwa madhara na umuhimu ya mambo hayo ili kulinda afya zao na kutimiza majukumu yao ipasavyo. Mafunzo hayo ya siku mbili yamefanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi jijini Dodoma kuanzia Novemba 29 hadi 30, 2024.
Akifungua mafunzo hayo Kaimu Msajili wa Bodi ya Nyama Tanzania Bw. John Chassama amewasisitiza watumishi hao kufuata miongozo ya utumishi wa Umma na kutii viongozi ili kuweza kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuepuka migongano isiyo ya lazima na kufanya kazi kwa ushirikiano.
Bw. Chassama amesema “tuishi kwa kufuata miongozo na tutii yote viongozi na wafawidhi wanayotuelekeza kwa kuwa wameteuliwa kushika nafasi hizo, hivyo tuwatii”.
Mtaalam kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Bi. Tezla Nkonya wakati akitoa elimu kwa watumishi hao kuhusu mapambano dhidi ya rushwa hasa mahala pa kazi aliipongeza Bodi hiyo kwa kutoa kibali kwa Wadau cha kufanya bishara ya nyama ndani ya saa 24 kwa kuwa hii inathibitisha utekelezaji wa majukumu katika bodi hiyo unavyofanyika kwa ufanisi mkubwa na hivyo kluzuia mianya ya rushwa.
Naye Dkt. Swai kutoka Hospitali ya Vichaa ya Milembe aliwaeleza watumishi hao namna afya ya akili inavyoweza kumbadili mtu na kufanya mambo yasiyofaa katika utekelezaji wa majukumu yake na kuwaasa kila mtumishi kulinda afya yake ya akili.
Vilevile, Dkt. Maghembe kutoka Kituo cha Afya Makole alitoa elimu juu ya VVU/UKIMWI na magonjwa yasiyoambukiza na kuwaeleza watumishi wa TMB umuhimu na namna ya kujilinda ili kuepuka magonjwa hayo kwani yanaweza kupunguza ari katika utekelezaji wa majukumu yao.
Aidha, watumishi waTMB walipata fursa ya kupima bure VVU/UKIMWI ili kutambua hali zao za kiafya ili kuwawezesha kuwalinda wenza wao.
Wakati huohuo, Bw. Chassama amewashukuru na kuwapongeza watumishi wa TMB kwa ushirikiano waliouonesha kwenye maandalizi ya kumuaga mtumishi mwenzao Bi. Elizabeth Shayo aliyestaafu utumishi wa Umma kwa mujibu wa sheria.