MUHTASARI WA UTAFITI WA BEI YA NYAMA
Imewekwa: 15 Apr, 2025
MUHTASARI WA UTAFITI WA BEI YA NYAMA

Katika kipindi cha kuanzia mwezi Oktoba mpaka Disemba 2024, kulishuhudiwa hali ya kuongezeka kwa bei ya rejareja ya nyama (nyama ya ng’ombe) katika maeneo mengi hapa nchini. Mwenendo huo wa kuongezeka kwa bei ya rejareja ya nyama kulipelekea bei ya wastani ya nyama kuwa Tsh 15,000 kwa baadhi ya maeneo kutoka wastani wa bei ya Tsh 7,000. Ongezeko hilo la bei lilisababisha/ lilipelekea Bodi ya Nyama Tanzania kufahamu sababu, madhara na fursa zinazoweza kuambatana na kupanda huko kwa kwa bei ya nyama ya ng’ombe.

Matazamio katika utafiti huo  ulikuwa ni kuja na mapendekezo yatakayosaidia kudhibiti hali hiyo, kupima ukubwa wa madhara yake na pia kumulika kama kunaweza kuwa na fursa zinazoambatana na mabadiliko hayo ya bei ya rejareja ya nyama.

Ili kuweza kupata matokeo yanayotarajiwa, utafiti huu ulitumia njia ya dodoso.Dodoso za aina mbili ziliandaliwa. Dodoso la  kwanza lililenga wadau mbalimbali kwenye mnyororo wa nyama, wakati la pili lilikuwa kwa ajili ya watu muhimu (key informants) ambao ama kwa uzoefu wao au taaluma zao wanaweza kuwa na taarifa ambazo zinaweza kuchangia katika kutoa majibu kwa malengo mahususi ya utafiti huo. Kwa hali hiyo, malengo mahususi ya utafiti yalikuwa pamoja na kuthibitisha kama kweli bei ya rejareja ya nyama imepanda katika maeneo mbalimbali hapa nchini; kuainisha sababu za kupanda kwa bei ya rejareja ya nyama na kuchambua madhara yatokanayo na kuongezeka kwa bei. Utafiti huu ulihusisha jumla ya wadau 509 kutoka katika mikoa 13 ya Tanzania bara.

Matokeo ya utafiti yamebainisha  kuwa katika kipindi cha kati ya mwezi Oktoba na Disemba 2024, bei ya nyama katika maeneo mbalimbali ya nchi ilipanda kutoka Shilingi za Kitanzania elfu saba (7,000/=) kwa kilo hadi kufikia Shilingi elfu kumi na tano (15,000/=) kwa kilo kwa baadhi ya maeneo. Aidha, kwa mujibu wa matokeo ya utafiti, kupanda kwa bei ya mifugo katika minada ndio kumetajwa kuwa sababu kubwa iliyopelekea kupanda kwa bei ya rejareja ya nyama. Kupanda kwa bei ya mifugo katika minada ni matokeo ya vitu vingi ikiwemo kuongezeka kwa mauzo ya nyama nje ya nchi ambayo yamepelekea kuongezeka kwa mahitaji ya mifugo na hivyo kupelekea bei kupanda. Aidha, mifugo mingi iliyo bora inayopelekwa minadani katika kipindi hicho ilitokana na unenepeshaji. Kupanuka kwa biashara ya  unenepeshaji kunaongeza gharama kwa wafugaji na hivyo wanavyopeleka minadanai nao wanauza kwa bei ya juu. Madhara ya kupanda kwa bei ya nyama kwa mujibu wa utafiti huo ni pamoja na kupungua kwa ulaji wa nyama katika ngazi ya familia, watu wamepoteza ajira ; uwezo wa watu kununua nyama umepungua na kusababisha mauzo ya nyama katika soko la ndani kushuka na kupelekea  uchumi wa wadau katika mnyororo wa biashara ya nyama kushuka. Kwa upande mwingine, wafugaji wamenufaika na ongezeko la bei ya mifugo. Aidha, kwa ujumla ongezeko hilo la mahitaji ya mifugo limeonesha na kufungua fursa ya ufugaji wa kibiashara.

Ili kukabiliana na hali hili kwa kipindi cha muda mfupi na muda mrefu, yafuatayo yanapendekezwa; Kuvutia vijana wengi kuingia kwenye ufugaji wa kibiashara utakaohusisha ufugaji wa mikataba na kuboresha upatikanaji wa mikopo kwa kundi hilo; Vilevile, kuweka mkazo kwenye upatikanaji wa huduma za ugani na kutoa elimu sahihi kuhusu kufanya unenepeshaji wa mifugo hasa kwa kutumia vyakula/ mimea/ masalia ya mazao yanayopatikana katika maeneo ambayo mafugaji wanapatikana. Pi ni muhimu maeneo ya wafugaji yatengwe na pia mbegu za malisho (majani) za aina mbalimbali kulingana na jiografia na hali ya hewa ya maeneo mbalimbali zipatikane. Aidha fursa ya uzalishaji wa vyakula vya mifugo kwa gharama nafuu kwa kutumia tekinolojia ya kisasa ikatumika ipasavyo ili kusaidia upatikanaji wa mifugo bora kwa bei nafuu muda wote wa mwaka. Hili litadaidia sana nyama na bidhaa zake zinazozalishwa nchini kuweza kushindana katika soko la ndani na nje ya nchi.