SEKTA BINAFSI ONGEZENI JITIHADA SOKO LA NYAMA NJE YA NCHI LIPO - DKT. MUSHI
Imewekwa: 11 Dec, 2023
SEKTA BINAFSI ONGEZENI JITIHADA SOKO LA NYAMA NJE YA NCHI LIPO - DKT. MUSHI

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt Daniel Mushi amezitaka sekta binafsi kuongeza juhudi katika biashara ya Mifugo na Nyama kwani soko la bidhaa hiyo nje ya nchi lipo.

 

Dkt. Daniel Mushi ameyasema hayo wakati akifungua Mkutano wa Wadau wa Tasnia ya Nyama na Mamlaka za Uwezeshaji Kibiashara kilichofanyika Desemba 07, 2023 jijini Dar es Salaam.

 

Dkt. Mushi amesema sekta  binafsi waongeze jitihada katika biashara ya Mifugo na Nyama ili mauzo ya Nyama nje ya nchi yazidi kile kiwango cha mwaka 2022/2023 cha tani 14,700.

 

Kuanzia Julai 2023 hadi Novemba 2023  kiasi Cha Tani 114 za Nyama zimesafirishwa nje ya nchi na kuingiza kiasi cha dola milioni 28, hivyo jitihada zikiongezeka kiasi hicho kitazidi kile cha mwaka jana, ameongeza Dkt. Mushi.

 

Mbali na hayo, Dkt Mushi amesema " Rais Samia amekuwa kipaumbele kufanya siasa za uchumi na kuwezesha kupatikana soko jipya la nyama la Saudi Arabia linalohitaji tani laki 7 kwa mwaka. Hivyo sekta binafsi ongezeni jitihada kupeleka nyama nje ya nchi kwani soko lipo"

 

Dkt. Mushi amesisitiza kuwa Serikali inafanya jitihada mbalimbali ikiwemo kuondoa baadhi ya tozo na kutengeneza mifumo ikiwemo MIMIS  ili kurahisisha utoaji wa huduma ikiwemo vibali vya biashara ya Mifugo na Nyama.

 

Awali, akimkaribisha Naibu Katibu Mkuu Mushi kufungua Mkutano huo Mwenyekiti  wa Bodi ya Nyama Tanzania Dkt. Clemence Tesha amewasihi Wadau hao kuwa wawazi na kutoa maoni yao ili kuweza kutatua changamoto zinazowakabili na kufanya biashara zao kwa ufanisi.

 

Aidha, Kaimu Msajili wa Bodi ya Nyama Bw. John Chassama amesema lengo la Mkutano huo ni pande hizo mbili za Wadau wa Tasnia ya Nyama na Mamlaka za Uwezeshaji Kibiashara kukutana ili kujadiliana namna ya kuboresha biashara ikiwemo kujua upungufu na changamoto zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi.

 

Vilevile, mmoja wa Wadau wa Tasnia ya Nyama Bw. Joseph Mwitatu ameiomba serikali iongeze machinjio ili kuboresha na kurahisisha suala la uchinjaji na biashara ya nyama kwa ujumla.