WAZIRI BASHIRU AWAHIMIZA WAUZA NYAMA NJE KUUNDA UMOJA IMARA
Imewekwa: 11 Feb, 2026
WAZIRI BASHIRU AWAHIMIZA WAUZA NYAMA NJE KUUNDA UMOJA IMARA

WAZIRI BASHIRU AWAHIMIZA WAUZA NYAMA NJE KUUNDA UMOJA IMARA

Wafanyabiashara wa nyama wanaouza bidhaa hiyo nje ya nchi wameshauriwa kuanzisha umoja thabiti utakaosaidia kurahisisha utendaji wa shughuli zao na kuwa chombo kikuu cha utatuzi wa changamoto zinazowakabili.

Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Bashiru Ali, Februari 11, 2026, katika hoteli ya Gerwill jijini Dodoma, wakati wa kikao maalum kilichoandaliwa na Bodi ya Nyama Tanzania (TMB) kilicholenga kujadili namna ya kuboresha sekta hiyo ili kuleta tija kwa taifa.

Mhe. Bashiru amesisitiza kuwa bila kuwa na umoja, itakuwa vigumu kwa wafanyabiashara hao kupiga hatua, hasa katika kutatua kero za usafirishaji na masoko ya kimataifa.

"Kikao hiki kiwe chimbuko la kuanzishwa kwa umoja wa wauza nyama nje ya nchi ulio imara. Harakisheni mchakato huu kwa kasi kwani bila umoja ni ngumu kufanikiwa," alisisitiza Waziri Bashiru.

Pia, Mhe. Bashiru amewasisitiza wafanyabiashara hao kuharakisha mchakato wa kuanzishwa kwa umoja kwa kasi na wasijisahau kwani bila umoja huo ni ngumu kwao kufanikiwa ikiwemo kutatua changamoto za usafirishaji wa nyama nje ya nchi.

Awali akielezea hali ya biashara ya nyama nje ya nchi Kaimu Msajili wa Bodi ya nyama Bw. John Chassama amesema Tanzania ina machinjio saba zenye ithibati ya kuzalisha nyama kwa ajili ya masoko ya nje zenye uwezo wa kuchinja ng’ombe kuanzia 100 hadi 1000 na mbuzi na kondoo 500 hadi 4500.

Bw. Chassama ameongeza kuwa katika kipindi cha kuanzia tarehe 1 Julai 2025 mpaka tarehe 30 Januari 2026, Tanzania imeuza jumla ya tani 9,325.8  za nyama nje ya nchi zenye thamani ya Dola za Kimarekani 39,459,370.71 na nyama iliyouzwa zaidi ni ya mbuzi.

Vilevile, wafanyabishara wa nyama nje ya nchi walipata nafasi ya kutoa maoni yao na kuelezea changamoto wanazokutana nazo wanaposafirisha nyama nje ya nchi ambapo wamelalamikia tozo wanazotozwa na baadhi ya mamlaka, uhaba wa upatikanaji wa malighafi, mawakala wa benki kutokuwepo minadani na kuwasababishia kutembea na pesa taslimu na hivyo kuhatarisha usalama wa fedha zao, umoja  wao utakapoanzishwa utawasaidia kuratibu bei ya bidhaa zao na pia wafanyabishara wadogo wadogo wawezeshwe kuwa katika mfumo rasmi wa biashara ya nyama nje ya nchi.

Akijibu hoja hizo, Waziri Bashiru amewahakikishia wafanyabiashara hao kuwa serikali imejipanga kuweka mazingira wezesha. Ametoa maelekezo kwa mabenki kuweka mawakala katika minada ya mifugo ili kuimarisha usalama wa fedha za wafanyabiashara na kuzuia uporaji.

Kikao hicho kimehudhuriwa na wafanyabishara ya nyama nje ya nchi kutoka kampuni 13 zilizopo mikoa mbalimbali ikiwemo Arusha, Dar es Salaam na Morogoro.