WATOA HUDUMA WA MADUKA YA NYAMA NA MACHINJIO WATAKIWA KUWAPA USHIRIKIANO WAKAGUZI
Imewekwa: 30 Apr, 2026
WATOA HUDUMA WA MADUKA YA NYAMA NA MACHINJIO WATAKIWA KUWAPA USHIRIKIANO WAKAGUZI

Mfawidhi wa Kanda ya Kati wa Bodi ya Nyama Tanzania Bw. John Kiboma amewataka watoa huduma wa maduka ya nyama na machinjio kutoa ushirikiano kwa wakaguzi kutoka Bodi ya Nyama Tanzania wanapotembelea katika maduka yao kwa ajili ya ukaguzi.

Bw. Kiboma ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya uuzaji na uandaaji wa nyama kwa watoa huduma wa maduka ya nyama na machinjio wa jijini Dodoma, Aprili 30, 2026.

Bw. Kiboma amesema “wakaguzi wanapofika katika maduka yenu wanakuja kwa ajili ya ukaguzi, hivyo msiwaone kama maadui bali muwape ushirikiano ili kuleta tija katika tasnia ya nyama”

Aidha, Bw. Kiboma amesema mafunzo hayo yana lengo la kuwakumbusha misingi sahihi ya uhudumu katika maduka ya nyama na machinjio pia kufuata taratibu sahihi za ufanyaji kazi katika maduka hayo.

Vilevile Afisa Mifugo wa Halmashauri ya jiji la Dodoma Bi. Delila Mlamka amewasisitiza washiriki wa mafunzo kuwa makini na elimu inayotolewa ili ikawe tija katika majukumu yao kwani watakapofanya makosa inaweza kuwasababishia kutozwa faini kwa makosa ya kawaida.

Bi. Delila aliongeza kwa kuwasisitiza wauza maduka ya nyama kuhakikisha wanauza nyama ya mnyama aliyechinjwa kwenye machinjio iliyosajiliwa kwani nyama hiyo huwa ni salama kwa kuwa kunakuwa na uhakika wa kufuata taratibu sahihi za uchinjaji wa mnyama.

Mbali na hayo, Wadau walioshiriki mafunzo hayo wameishukuru Bodi ya Nyama kwa kuwapatia elimu hiyo kwani wamejua namna bora ya kutunza nyama na namna ya kuongeza thamani katika zao la nyama ikiwemo kutolaza nyama na badala yake kutengeneza soseji kwa nyama iliyobakia buchani kwa siku hiyo.

Wahudumu wa maduka na nyama na machinjio wamepata mafunzo juu ya muongozo wa uuzaji wa nyama na bidhaa zake kwenye maduka ya nyama na namna ya kuongeza thamani katika bidhaa ili kuweza kuboresha biashara ya nyama.