Wadau wa tasnia ya nyama nchini wametakiwa kuzingatia na kushiriki kwa vitendo mafunzo wanayopewa na Bodi ya Nyama Tanzania kuhusu miongozo ya ufanyaji wa biashara ya nyama ili kuhakikisha uzalishaji wa nyama unaboreshwa na kupata nyama bora na salama.
Hayo yamesemwa na Dkt. Nassoro Mopei ambaye ni Mshauri wa mifugo mkoa wa Dar es Salaam aliyekuwa mgeni rasmi katika mafunzo ya siku mbili kwa wadau wa tasnia ya nyama kuanzia Juni 2 hadi 3, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo hayo.
Dkt. Mopei amesema “wadau msiwe washiriki tu bali mshiriki kwa vitendo ili lengo la mafunzo lifikiwe na kuboresha sekta ya mifugo katika kuchangia pato la taifa kwani rasilimali kubwa ya mifugo iliyopo nchini haiendani na mchango wake katika pato hilo”
Dkt. Mopei ameongeza kuwa hali ya ukuaji wa uchumi kama ilivyoelezwa na benki ya dunia inaonyesha uchumi wa Tanzania unakua lakini serikali ikiweka mkazo zaidi katika mifugo uchumi utakuwa zaidi kwa kuwa sekta ya mifugo inagusa maisha ya watanzania.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Afisa Mfawidhi Kanda ya Mashariki kutoka Bodi ya Nyama Tanzania Bw. Joseph Kulwa amesema mafunzo kwa watoa huduma wa maduka ya nyama, machinjio na viwanda vya nyama yana lengo la kukuza uelewa kwa wadau hao ili kuongeza soko la ndani na nje ya nchi.
Bw. Kulwa aliongeza kuwa mafunzo haya yatawawezesha wafanyabiashara ya nyama kuelewa miongozo na taratibu zitakazowawezesha kupata nyama bora na salama ili kukidhi vigezo vya soko la nyama hasa la nje.
Aidha, Bw. Kulwa amesema kuwa Bodi ya Nyama inatarajia baada ya wadau wa tasnia ya nyama kupata mafunzo mdau mmoja mmoja kwa namna yake atapiga hatua na sekta ya nyama pia itapiga hatua katika kukuza uchumi wa nchi.
Naye mdau wa tasnia ya nyama Bw. Maulid Mikidadi ameishukuru Bodi kwa elimu inayowapatia na kuiomba serikali iwekeze zaidi katika kuwawezesha mitaji ili waweze kukidhi vigezo na kufikia soko la kimataifa . Akitoa uzoefu wake katika biashara ya nyama Bw. Maulidi amewaasa wafanyabishara hiyo kuchagua maeneo rahisi kufikika kufungua biashara zao ambapo itawawezsha kupata wateja kwa urahisi.
Mafunzo haya yaliyoandaliwa na Bodi ya Nyama Tanzania hutolewa nchini kote kwa lengo la kuwaelimisha wadau wa tasnia ya nyama kuzalisha na kuuza nyama iliyo bora na salama na kukuza soko la bidhaa hiyo muhimu.

