AFYA, LISHE NA MBEGU BORA NI MSINGI WA UZALISHAJI WA MIFUGO NA KUKIDHI MAHITAJI YA SOKO
Uzalishaji wa mazao bora ya mifugo unategemea lishe, mbegu na afya bora ili kuweza kukidhi hitaji la masoko ya mifugo na mazao yake ndani nan je ya nchi.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Kakurwa wakati akifungua kikao cha wadau katika mnyororo wa thamani ya nyama kujadili fursa ya kufunguka kwa soko la Mauritius. Kikao hicho kimefanyika jijini Dodoma Novemba 20, 2026.
Dkt. Bashiru amewataka wafugaji kuwekeza nguvu zaidi kwenye lishe za mifugo ikiwemo kuwapatia malisho sahihi na ya kutosha ikiwemo maji na chumvi ili kuweza kuzalisha mifugo yenye afya bora itakayowezesha kupata masoko kwa urahisi na kwa bei nzuri.
Akizungumzia upatikanaji wa soko jipya la wanyama hai la Mauritius, Dkt. Bashiru amesema Dira ya 2050 inayolenga kuimarisha mchango wa sekta ya mifugo katika ukuaji wa uchumi wa Taifa inataka tusijivunie kupata soko la wanyama hai bali tuone namna ya kuongeza thamani kwa mifugo hiyo na kupata masoko ya bidhaa za mifugo ikiwemo manyoya, ngozi, kwato, macho na pembe .
Vilevile , Dkt. Bashiru ametaka mashamba ya malisho mazuri yasajiliwe ili kutambulika na kuwezesha wafugaji kupata sehemu sahihi ya kupata malisho kwa ajili ya mifugo yao na pia kuwe na mfumo unaokidhi mahitaji ya wafugaji ikiwemo upatikanaji wa taarifa sahihi za mifugo.
Aidha, Dkt Bashiru amesema serikali ya awamu ya sita ina lengo la kufikia tani 50,000 ya nyama kuuzwa nje ya nchi ifikapo 2030 ambapo kwa sasa Tanzania inauza tani 15,000 nje ya nchi kutoka tani 1000 zilizokuwa zikiuzwa wakati awamu hiyo ilipoingia madarakani.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Mhe. Petro Magoti ameahidi kutoa eneo la ranchi, machinjio, malisho na minada katika wilaya hiyo ili kuwawezesha wafugaji kuwa na eneo la uhakika kwa ajili ya kufuga na kuzalisha mazao yaliyo bora.
Pia, Mhe. Magoti amewasisitiza wafanyabiashara ya mifugo na mazao yake kuchangamkia soko la Mauritius ili kuweza kukuza biashara zao.
Awali akimkaribisha Dkt. Bashiru kufungua kikao hicho Naobu Katibu Mkuu (mifugo) Dkt. Fabian Madele amesema kikao hicho kimehusisha wafugaji, chama cha wafugaji, wasindikaji wa mazao ya mifugo, wasafirishaji wa nyama nje ya nchi na wamiliki wa mashamba ya mifugo ikiwa na lengo la kujadili upatikanaji wa soko jipya la Maurutius.

