
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Edwin Mhede amewataka wafugaji nchini kuwekeza kwenye mbinubora za ufugaji ili kushusha gharama za ufugaji na kuongeza tija ili kuwa na bei himilivu kwa walaji.
Dkt. Mhede ameyasema hayo wakati akifungua maonesho ya tisa ya ndege wafugwao ikiwemo kuku, katika ukumbi wa Mlimani city jijini Dar es Salaam Oktoba 10, 2025.
Dkt. Mhede amesema “mbinu bora za ufugaji zitashusha gharama au kuongeza tija ili kuwa na bei himilivu kwa walaji na kuongeza mzunguko wa ulaji kuku kwani ulaji wa nyama na mayai ya kuku ni mdogo kutokana na bei zake”.
Naibu Katibu Mkuu huyo ameongeza kuwa mtazamo wa serikali kwa sasa ni kuwa sekta ya ufugaji kuku ni miongoni mwa sekta muhimu kwa lishe bora hivyo sekta za mifugo zitoe takwimu sahihi za mahitaji ya chakula cha mifugo ikiwemo ndege wafugwao ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula cha kuku.
Vilevile Dkt Mhede amesema sekta ya ufugaji imeshapasua anga za kimataifa na hii inaonyesha kukua kwa sekta hii hivyo amewashauri wafugaji kukaa pamoja na washiriki kutoka nje ya nchi na kuona namna ya kuikuza zaidi tasnia ya ufugaji wa ndege wafugwao.
Aidha, Dkt. Mhede ameahidi kufanyia kazi changamoto za wafugaji kuku ikiwemo kudhibiti vifaranga kutoka nje ya nchi ili kuzuia magonjwa ikiwemo mafua makali. Pia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Bodi ya Nyama Tanzania watafanya utafiti ili kuona namna ya upatikanaji wa machinjio ya kuku.
Pia, Dkt. Mhede amesema kuwa hadi sasa asilimia 98 ya kuku wameshachanjwa tangu kuzinduliwa kwa zoezi la uchanjaji na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mwezi Juni 2025.
Awali akimkaribisha Naibu Katibu mkuu kuzungumza na wafugaji Kaimu Msajili wa Bodi ya Nyama Tanzania Bw. John Chassama amesema sekta ya ufugaji ni sekta inayokuwa kwa kasi, hivyo amewashukuru na kuwapongeza wafugaji kujitokeza kwa wingi ili kujifunza mambo mbalimbali yahusuyo ufugaji.
Naye Mwenyekiti wa chama cha ufugaji kuku na ndege wafugwao Bi. Mwamvua amesema tasnia ya ufugaji kuku na ndege wafugwao imekuwa ikikua na uwekezaji mkubwa umewekwa na hivyo kupunguza utegemezi wa bidhaa za kuku kama mayai kutoka nje.
Maonesho haya hufanyika kila mwaka na washiriki wamekuwa wakiongezeka kutoka mataifa mbalimbali. Katika maonesho ya 9 Washiriki 53 wameshiriki kutoka ndani na nje ya nchi zikiwemo nchi za Malawi, Kenya, Afrika Kusini, India, Canada, Ujerumani na Ufaransa.