BODI YA NYAMA YAONYA WAUZAJI WA NYAMA WANAOPULIZA DAWA YENYE SUMU KWENYE MABUCHA
Imewekwa: 27 Mar, 2024
BODI YA NYAMA YAONYA WAUZAJI WA NYAMA WANAOPULIZA DAWA YENYE SUMU KWENYE MABUCHA

(Stori kwa hisani ya Mbeyapresstv.blogspot,com)

Bodi ya Nyama Tanzania (TMB) Nyanda za Juu Kusini imepiga marufuku wauzaji wa bucha za nyama kupuliza dawa zenye sumu mabuchani ili kulinda afya za walaji.

Ofisa Mfawidhi wa Bodi ya Nyama Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Dkt. Mpoki Alinanuswe amesema jana mkoani hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema kitendo cha wauzaji kupuliza sumu kunaweza kuleta madhara makubwa kwa walaji huku akibainisha watu 10 wamechukuliwa hatua katika Mikoa ya Mbeya na Songwe.

“Tulifanya ukaguzi maalum katika maeneo ya machinjio, mabucha, magari, na pikipiki zinazotumia kusafirisha nyama katika maeneo mbalimbali katika Mikoa hiyo na kubaini changamoto na tayari tumetoa maelekezo” amesema.

Wakati huo huo, amewataka wauzaji wa nyama kutekeleza agizo la kuwataka kutumia vifaa vya kisasa kucharanga nyama na kuachana na tabia ya kutumia magogo ambayo sio salama kwa afya za walaji.

Dkt. Mpoki ameongeza kuwa “Tutaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara lengo ni kuhakikisha watumiaji wanakuwa salama sambamba na wafanyabiashara ya bucha kuzingatia kanuni za afya".

Amesema katika zoezi la ukaguzi walilofanya katika maeneo ya machinjio wamebaini kutokuwepo kwa mazingira rafiki kwa baadhi ya machinjio kutokana na usimamizi usio mzuri wa Halmashauri.

Muuza bucha ya nyama eneo la Soweto Jijini hapa Bw. Athanas Nassoro ameomba elimu itolewe na sio kwamba wanafanya kwa bahati mbaya lengo ni kuondoa wingi wa nzi wanaozaliana.