MUUZA DUKA LA NYAMA ASIYE NA CHETI CHA MAFUNZO HATORUHUSIWA KUTOA HUDUMA
Imewekwa: 02 May, 2025
MUUZA DUKA LA NYAMA ASIYE NA CHETI CHA MAFUNZO HATORUHUSIWA KUTOA HUDUMA

Bodi ya Nyama Tanzania (TMB) yatoa mafunzo kwa watoa huduma katika maduka ya nyama kwa lengo la kuwawezesha kutoa huduma bora ili kumlinda mteja na kuhakikisha biashara inakua.

Mafunzo hayo ya siku moja yanategemewa kukuza uelewa kwa watoa huduma hao juu ya kutumia vifaa sahihi vya mabuchani ikiwemo nondo za aluminium, gogo la plastiki n.k. Mafunzo hayo yamefanyika Aprili 30, 2025 jijini Dodoma.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Afisa Mifugo kutoka TMB Bw. John Kiboma amesema wanatarajia baada ya mafunzo hayo watoa huduma waliopata mafunzo watakuwa ni mabalozi wazuri kwa wengine ambao hawakufanikiwa kushiriki mafunzo hayo ambayo yanatarajiwa kufanyika wilaya zote nchini.

Naye Daktari wa mifugo wa Halmashauri ya jiji la Dodoma Dkt. Herman Nicholaus amesema mafunzo hayo ni muhimu ili kuwawezesha wahudumu hao na wafanyabiashara ya nyama kiujumla kutambua mambo mbalimbali ikiwemo magonjwa ya mifugo.

Pia, Dkt. Herman alitoa wito kwa wafanyabiashara ya nyama kuzingatia afya za walaji kwa kuhakikisha bidhaa zao ni salama.

Vilevile, Bi. Cecilia Andrea mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo amesema ”mafunzo haya ni muhimu kwani tunaelekezwa juu ya usafi katika biashara ya maduka ya nyama ili kuweza kulinda afya za walaji ambao ndio wateja wetu”.

Aidha, Bi. Cecilia alitoa wito kwa watoa huduma katika maduka ya nyama ambao hawajahudhuria mafunzo wasiwe wanapuuza wanapopewa taarifa juu ya ushiriki kwenye mafunzo hayo muhimu ili kuboresha ufanyaji kazi wao.

Mafunzo haya ni ya awamu ya tatu  na yanafanyika kila mwaka ili kuboresha na kukuza biashara ya nyama.