Usajili

Usajili wa Wadau wa Tasnia ya Nyama

 

1. UTANGULIZI

Tasnia ya nyama hapa nchini inasimamiwa na Sheria ya Nyama Na. 10 ya Mwaka 2006. Sheria hii ilitungwa kutokana na kuwepo kwa ombwe katika usimamizi wa tasnia ya nyama baada ya kuvunjwa kwa mamlaka ya kusimamia na kuendeleza mifugo na mazao yake (Livestock Development Authority - LIDA) mwanzoni mwa miaka ya 1980. Vile vile kumekuwepo na hitajio la nyama bora na salama katika soko la ndani na nje ya nchi.

Ili kusimamia utekelezaji wa sheria ya Nyama Na. 10 ya Mwaka 2006 Bodi ya Nyama Tanzania iliundwa chini ya kifungu 9 (1) kwa lengo la kuweka misingi thabiti ya kuendeleza uzalishaji, usindikaji, biashara ya mifugo, nyama na mazao yake inayozingatia ubora na viwango ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi. Aidha, katika kutekeleza majukumu hayo Bodi haina budi kushirikiana na wadau mbalimbali zikiwemo Mamlaka za Serikali za Mitaa, hivyo Bodi imeandaa kanuni na miongozo ya ukaguzi, upangaji wa madaraja ya mifugo na nyama na usajili wa wadau wa tasnia ya nyama ili kuelekeza wadau katika kutekeleza majukumu yao kwa mujibu ya sheria. Ili kutekeleza usajili ni dhahiri kuwa ukaguzi ndio ufunguo wa utambuzi na usajili wa wadau wa Tasnia ya Nyama.

2.USAJILI WA WADAU WA TASNIA YA NYAMA

2.1 Lengo la Usajili

Kuwezesha wadau kushiriki kikamilifu katika kuendeleza tasnia ya nyama kuanzia kwenye uzalishaji, usindikaji, biashara ya mifugo, nyama na mazao yake. Vile vile inawezesha wadau kupatiwa huduma mbalimbali zikiwemo taarifa muhimu za tasnia na kuunda mtandao baina yao.

2.2 Wadau na Maeneo Yatakayosajiliwa

Watakaosajiliwa na kutambuliwa ni watu binafsi, taasisi, vyama vya kijamii kampuni na maeneo yanayotumika katika uzalishaji wa mifugo, katika hatua mbalimbali za mnyororo wa thamani wa zao la nyama kibiashara. Wadau na maeneo hayo ni pamoja na:-

 • Wafugaji wa mifugo wa nyama wa aina zote kwa ajili ya biashara;
 • Vyama vya wadau vinavyotambulika kisheria;
 • Minada ya mifugo
 • Dalali wa Mifugo
 • Mwendesha Minada
 • Mfanyabiashara wa mifugo hai ndani na nje ya nchi, nyama (maduka ya Nyama) na mazao ya nyama
 • Wakala wa biashara ya nyama na mazao ya nyama
 • Watengenezaji na waagizaji wa mashine za uzalishaji wa nyama na pembejeo
 • Machinjio na Viwanda vya Nyama na bidhaa za Nyama
 • Waendesha matamasha ya Nyama
 • Waingizaji na wauzaji wa nyama ndani na nje ya nchi.

3. VIGEZO VYA USAJILI

3.1 Mfugaji/Mmiliki wa shamba la mifugo

 • Awe na eneo la ufugaji linalotambuliwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na awe na anuani ya kudumu
 • Awe mfugaji anayefuga kwa lengo la biashara
 • Awe analisha mifugo yake vyakula vinavyotambuliwa na Sheria za Magonjwa ya Wanyama Na. 17 ya mwaka 2003 na Maeneo ya Malisho na Vyakula vya Mifugo Na. 13 ya mwaka 2010
 • Awe anamilki mifugo ya nyama isiyopungua ng’ombe 5, mbuzi 20, kondoo 20 au nguruwe 15 kwa mwaka au kuku 1000 kwa wakati mmoja

3.2Minada ya Mifugo

 • Mnada wa awali, upili au mpakani ulioanzishwa kisheria
 • Mnada unaokidhi mahitaji ya miundombinu ikiwemo mizani, eneo la kupumzisha mifugo, kiringe cha kunadishia kama ilivyoelekezwa kwenye Kanuni Na. 6 ya kuanzisha, kusimamia na kuendesha minada ya mwaka 2010.

3.3 Msimamizi wa Mnada

 • Awe mwenye elimu ya kiwango kisichopungua Astashahada ya uzalishaji na afya ya mifugo kwa minada ya awali na Stashahada ya uzalishaji wa mifugo kwa minada ya upili na mipakani
 • Awe ameteuliwa na mamlaka husika.

3.4 Dalali

 • Awe na leseni ya udalali
 • Awe ameomba kazi ya udalali katika mamlaka husika inayomiliki mnada na kukubalika
 • Awe na uzoefu wa biashara ya mifugo.

3.5 Mfanyabiashara wa Mifugo hai ndani na nje ya nchi

 • Awe na anuani
 • Awe analipa kodi za serikali
 • Awe na leseni ya biashara.

3.6 Vyama na Vikundi vya Wadau

Vyama vitakavyosajiliwa ni pamoja na vyama na vikundi vya wafugaji, wafanyabiashara, wasindikaji, walaji, wauza pembejeo, wauzaji na waangizaji nyama, bidhaa zake na pembejeo nje ya nchi.

Vyama hivyo vinatakiwa kuwa na sifa zifuatavyo:-

 • Viwe vimesajiliwa kisheria
 • Viwe na Katiba
 • Viwe na ofisi yenye watendaji na inayofanya kazi
 • Viwe na njia mbalimbali za kuongeza mapato na akaunti benki
 • Viwe na wanachama hai
 • Viwe hai na vinavyofanya mikutano kwa mujibu wa katiba.

3.7 Wadau wengine watakaotambuliwa

Wadau wengine na maeneo yao wanaotakiwa kutambuliwa ni pamoja na:-

 • Machinjio
 • Wasindikaji
 • Wasambazaji wa nyama na mazao yake na
 • Waagizaji na wauzaji wa nyama na mazao ya nyama nje ya nchi

3.8 Utaratibu wa Kusajili

Utaratibu wa kusajili wa wadau na maeneo ya uzalishaji mifugo utazingatia mambo yafuatayo:-

 • Mwombaji mwenye sifa ataomba usajili kwa kujaza fomu maalum zinazopatikana katika ofisi zote za Mifugo zilizopo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na Ofisi ya Msajili wa Bodi ya Nyama Tanzania kwa gharama ya shilingi 20,000/-ambazo hazitarejeshwa
 • Mwombaji atajaza fomu hizo na kuzirudisha kwenye ofisi ya Afisa wa Serikali aliyeteuliwa kutekeleza majukumu ya Bodi katika eneo husika
 • Afisa wa eneo husika atakagua eneo na nyaraka muhimu na kujaza mapendekezo yake kwenye kwenye fomu ya mwombaji
 • Fomu hizo zitatumwa kwa Msajili wa Bodi ambaye atazihakiki kabla ya kuziwasilisha kwenye Kikao cha Bodi kwa maamuzi ya usajili
 • Bodi itaidhinisha au kukataa usajili wa mwombaji endapo atakidhi au hatakidhi vigezo vya usajili
 • Mwombaji atakayepata usajili atalipa ada ya usajili kulingana na shughuli zake na atapewa cheti cha usajili kitakacholipiwa ada ya kila mwaka.
 • Umiliki wa cheti cha usajili hautahamishiki
 • Bodi inaweza kufuta usajili kabla ya muda wake kwisha, endapo mdau atashindwa kukidhi vigezo vya usajili
 • Endapo kutakuwa na mabadiliko ya anuani, maombi ya kubadilisha cheti yatumwe katika ofisi za Bodi ndani ya siku 45.
 • Endapo cheti cha usajili kitapotea au kuharibika, mdau atoe taarifa kwa Msajili wa Bodi kwa kuwasilisha ushahidi wa vielelezo vya upotevu kutoka polisi. Bodi ikiridhika na ushahidi itatoa nakala iliyoidhinishwa (certified copy) kwa gharama ya shilingi 20,000/=.